+255(0)232604380/1/3/4 | P.O. Box 9, Mzumbe, Morogoro - Tanzania

Jul 19, 2023 313times

MAKAMU MKUU WA CHUO ATETA NA WANACHUO WATARAJIWA KUJIUNGA NA CHUO KIKUU MZUMBE.

Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Mtiva wa Kitivo Cha Sheria cha Chuo hicho Dkt. Saraphina Bakta, amezungumza na Wanafunzi wa shule za Sekondari na Wananchi waliotembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe ili kujifunza shughuli za kitaaluma zinazotolewa na Chuo hicho katika Maonesho ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Akitoa huduma kwa Wanafunzi na Wananchi waliofika bandani hapo kwa nyakati tofauti Dkt.Bakta ameendelea kutoa wito kwa watu wote wanaotarajia kujiunga na masomo ya Elimu ya Juu kwa Mwaka wa masomo 2023/2024, kutembelea katika banda la Chuo Kikuu Mzumbe ili kuzijua zaidi kozi zitolewazo na Chuo hicho kuanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili pamoja na Shahada ya Uzamivu .
Akizungumza na Wanafunzi wa Kidato Cha Sita kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Kisutu waliotembelea banda la maonesho la Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Bakta amewapongeza Wanafunzi hao kwa kujitambua na kuanza mapema harakati za kutafuta taarifa kuhusu vyuo wanavyotaka kujiunga na kuwahakikishia kuwa Chuo Kikuu Mzumbe ni Chuo sahihi kwao kutokana na utajiri wa kozi ilizonazo kuendana na Tahsusi (Combination) wanazosoma sasa huku akitanabaisha upatikanaji wa miundombinu muhimu yakiwemo mabweni na mazingira salama ya kujifunzia kwa Wanafunzi wote hususani wa kike
“Nawapongeza kwa kuja kutembelea banda letu ili kufahamu kozi zinazotolewa na chetu pamoja na sifa za kujiunga.
Chuo Kikuu Mzumbe tunazo kozi nyingi na tumebobea kwenye Sheria, Utawala, Uhasibu ,Sayansi na Teknolojia,Uendeshaji wa Mifumo ya Afya,Fedha ,Biashara pamoja na masoko . Tunawakaribisha sana mtakapohitimu kidato cha sita muweze kujiunga na chuo chetu, pia mkawe mabalozi katika kuhamasisha wanafunzi wenzenu kujiunga Chuo hiki kwani ni Chuo bora”Alisema Dkt Bakta
Aidha Dkt. Bakta amesisitiza kuwa huduma ya kutuma maombi ya kujiunga na Chuo Kikuu Mzumbe ni rahisi sana kwani maombi hutumwa kwa njia ya mtandao kwa kozi zote zinazotolewa katika Kampasi tatu ambazo ni Kampasi kuu iliyopo mkoa wa Morogoro, Ndaki ya Mbeya pamoja na Ndaki Dar es Salaam (Tegeta na Upanga)
Azungumza kwa niaba ya Wanafunzi wenzake dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisutu, Jesca Mulla amekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwapa uelewa mapema wa kozi zinazotolewa na Chuo hicho pamoja na sifa zinazotakiwa ili kuweza kujiunga na elimu ya juu.
“Tunashukuru sana kwa Chuo Kikuu Mzumbe kuweza kutuelimisha kuhusu vigezo vya kujiunga na elimu ya juu imekuwa bahati kwetu kwani tuna muda wa kujiandas ili tufikie vigezo lakini pia tunakwenda kuwapa taarifa wanafunzi wenzetu waliomaliza waje kufanya maombi katika Chuo hiki kwani kimekuwa kikitoa elimu Bora" amesema Mulla.
Maonyesho ya 18 ya Vyuo Vikuu nchini yameanza Julai 17, na yataendelea hadi Jumamosi tarehe 22 Julai 2023, katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
 
Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Mtiva wa Kitivo Cha Sheria cha Chuo hicho Dkt. Saraphina Bakta,
akimkabidhi zawadi ya kikombe Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisutu, Jesca Mulla.
 
Mratibu za Udahili Chuo Kikuu Mzumbe,Dkt Michael Mangula(katikati) akisisitiza jambo Kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisutu walipotembelea
Banda la Chuo Kikuu Mzumbe.(kulia) ni Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Mtiva wa Kitivo Cha Sheria cha Chuo hicho Dkt. Saraphina Bakta.
 
Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Mtiva wa Kitivo Cha Sheria cha Chuo hicho Dkt. Saraphina Bakta, akiwapa vipeperushi ya
kuonyesha kozi za Mzumbe Kwa wanafunzi wa Kidato Cha sita wa Shule ya Sekondari Kisutu ya Jijini, Dar es Salaam
Go to top
JSN Educare is designed by JoomlaShine.com | powered by JSN Sun Framework