+255(0)232604380/1/3/4 | P.O. Box 9, Mzumbe, Morogoro - Tanzania

Jun 06, 2023 258times

BODABODA WAPONGEZA CHUO KIKUU MZUMBE KWA KUWAPATIA MAFUNZO NA KUJALI USALAMA

Umoja wa Waendesha Pikipiki maarufu kama bodaboda kata ya Mzumbe wamekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kujali usalama wao na abiria wanaowabeba hususani Wanafunzi na Wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya Sheria na usalama barabarani pamoja na wajibu wa kujilinda na makosa ya jinai

Akizungumza kwa niaba ya umoja huo mara baada ya mafunzo hayo yaliyoratibiwa na  kituo cha msaada wa kisheria cha kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe na kufanyika katika ukumbi wa Maekani uliopo Kampasi Kuu Morogoro, Mwenyekiti wa bodaboda kata ya Mzumbe Bw.David Msambaa ameshukuru na kukipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa  kuwapatia mafunzo hayo na kueleza kuwa elimu hiyo imewasaidia kufahamu mambo mengi kuhusu Sheria za barabarani na kwamba itawaepusha na makosa waliyokuwa wakiyafanya bila kujua hapo awali.

“Mafunzo haya ni msaada mkubwa kwetu kwani tumegundua tulikuwa tunafanya makosa mengi bila kujua, tunashukuru sana Wataalamu wa Chuo Kikuu Mzumbe, tupo tayari kuyaishi tuliyofundishwa na kuendeleza uhusiano mzuri na ushirikiano baina yetu na chuo hata kwa masuala mengine ya kimaendeleo”. Alisema Mwenyekiti huyo

Awali akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe Dkt.Seraphina Bakta alisema kuwa Waendesha bodaboda wana mchango mkubwa sana kwa Jamii, familia na uchumi wa nchi  kwani ndiyo usafiri rahisi na wa haraka unaotumiwa na watu wengi  na hivyo ni muhimu wakaelimishwa na kufuata Sheria nyakati zote ili jamii iondokane na dhana ya kuwa waendesha bodaboda ni Wahalifu

Naye Afisa Usalama wa Chuo Kikuu Mzumbe ASP Mkaine Man, amesema kwamba Chuo kitaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa Wanajumuiya wote  wakati huo huo kikiweka mazingira salama kwa bodaboda  wote kufanya kazi zao bila usumbufu ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitambulisho maalum ‘reflectors’ zenye namba ili kudhibiti vitendo vya kihalifu

Kwa upande wake Mratibu wa kituo cha msaada wa kisheria na Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu Mzumbe Wakili Bernadetha Iteba amesema kuwa, mafunzo hayo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa chuo katika kuihudumia jamii hususani makundi maalum na kusisitiza kuwa bodaboda ni kundi muhimu lenye muingiliano mkubwa na Wanajumuiya wa chuo hivyo ni vyema wakazielewa vyema Sheria za barabarani na kutambua wajibu wao wa kujilinda na makosa ya jinai ili kuwaepusha na vitendo vinavyoweza kuwapelekea kuingia kwenye mgogoro wa kisheria ikiwemo kujihusisha kimapenzi na Wanachuo walio na umri chini ya miaka 18.

Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe Dkt.Seraphine Bakta akifungua mafunzo ya Bodaboda yaliyoendeshwa na kituo cha msaada wa kisheria.

Mratibu wa Kituo cha Msaada wa Kisheria na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Wakili Bernadetta Iteba akiwasilisha mada

Mwakilishi wa kituo cha Polisi Mzumbe CPL Alawu akitoa mafunzo kwa Waendesha Bodaboda wa kata ya Mzumbe.

 

Afisa Usalama wa Chuo Kikuu Mzumbe ASP Mkaine Man akitwasilisha mada katika mafunzo hayo

Baadhi ya Waendesha Bodaboda wa kata ya Mzumbe wakifuatilia mafunzo ya Sheria na usalama barabarani yaliyoratibiwa na Chuo Kikuu Mzumbe.

Washiriki wakifuatilia mafunzo hayo kwa umakini

Go to top
JSN Educare is designed by JoomlaShine.com | powered by JSN Sun Framework